Idara ya afya kaunti ya Kilifi imetenga kima cha shilingi milioni tano katika bajeti ya mwaka 2022/2023, ili kutekeleza ujenzi wa kitengo cha wagonjwa kufanyiwa vipimo vya X-ray, katika hospitali ya Bamba eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya afya katika bunge la kaunti ya Kilifi Edward Kazungu, wizara ya afya kaunti ya Kilifi inafahamu kuhusiana na changamoto zinazokabili hospitali ya Bamba eneo bunge la Ganze na imeendelea kujitahidi kutatua changamoto hizo.
Akizungumza katika kikao cha bunge wakati akitoa ripoti ya kamati ya afya kuhusiana na shughuli za kuboreshwa kwa huduma za afya katika kituo hicho cha afya, mwenyekiti huyo ambaye pia ni mwakilishi wa wadi ya Mwanamwinga kaunti ya Kilifi, amesema kando na hayo pia wametenga kima cha shilingi milioni mbili ili kununua vifaa hitajika vya matibabu katika taasisi hiyo ya afya.
Aidha, amesisitiza kuwa idara ya afya kaunti ya Kilifi itatilia mkazo utekelezaji wa miradi hiyo na kusema ipo haja ya serikali ya kaunti, kuongeza mgao unaotengewa sekta ya afya kaunti ya Kilifi, katika mwaka ujao wa kifedha ili kukidhi mahitaji ya hospitali za kaunti.
WIZARA YA AFYA KAUNTI YA KILIFI KUTENGA SHILINGI MILIONI TANO

