NAIBU GAVANA WA KAUNTI YA KILIFI AWAPONGEZA WALIMU AMBAO WANAFUNZI WAO WALIFANYA VYEMA KWENYE MITIHANI YA KITAIFA

Naibu gavana wa kaunti ya Kilifi Flora Chibule amepongeza hatua ya mbunge wa eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi, Amina Mnyazi kuandaa hafla ya kuwazawadi walimu bora baada ya wanafunzi wao kufanya vyema kwenye mitihani ya KCPE na KCSE katika shule za msingi na upili zilizopo eneo bunge la Malindi.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuwazawadi walimu, Chibule amesema bidii ya walimu katika kuwaelemisha wanafunzi ndio huchangia kwa matokeo bora kwa wanafunzi wanapofanya mitihani yao ya kitaifa.
Kwa mujibu wa Chibule, sasa serikali ya kaunti ya Kilifi itachukua jukumu la kuandaa hafla sawia na hiyo, ili kuwapongeza walimu watakaowasadia wanafunzi kufanya vyema katika mitihani ya kitaifa mwaka huu wa 2023.
Kwa upande wake waziri wa elimu wa kaunti ya Kilifi Clara Chonga, amewataka walimu kuchukuwa jukumu la kuhakikisha wanafunzi wa familia zisizojiweza kifedha, wanaelekezwa jinsi wataweza kupata ufadhili ili waendeleze masomo yao.