Bao la fowadi Samuel Chikola ndio bao la pekee lililosababisha vijana wa furunzi fc wikendi ilopita kusajili ushindi dhidi ya klabu ya Simba Apparel katika mechi ilochezwa dimbani Alaskan mjini Malindi kaunti ya Kilifi.
Ushindi huo wa bao 1-0 unaifanya Furunzi Fc ya mkufunzi Nero Chishenga sasa kupanda hadi nafasi ya tano wakiwa na alama 11 katika ligi ya daraja la pili kitaifa.
Katika kaunti ya Lamu bao la Ali Yaya liliwapa Sango Sportiff wa kaunti ya Tana River ushindi bao 1-0 dhidi ya Deep Sea katika dimba la Sposi.
Matokeo hayo sasa yanafanya Sango kupanda hadi nafasi ya 9 ligini wakiwa na alama 8.
Klabu ya Kantonga ya Taita Taveta ilizawadiwa alama tatu na mabao mawili kwa mantiki ya Beach Bay wageni wao kukosa kuheshimu ratiba.
Yanga ya Mkufunzi Collins Omondi ilipiga sare ya bao 1-1 dhidi ya Ashton Rangers katika kaunti ya Mombasa huku vijana wa Juma Kalato Omax FC ikilazimishwa sare tasa dhidi ya wenyeji wao Shimanzi fc.
Samburu Lions nao walisajili ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mariakani FC wakati Inter Dabaso wakiwa nyumbani kwao wakitandika Sparki Youth kichapo cha mabao 4-2, Maji Bombers wakipoteza kwa kichapo cha bao moja komboa ufe katika dimba lao la nyumbani Ziwani Youth.

