KLABU YA VIHIGA YAPIGWA NA AFC LEOPARDS, MKUFUNZI GEORGE OWOKO ALALAMA

Mabingwa mara 12 wa ligi kuu ya KPL, AFC Leopards jana walisajili ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vihiga Bullets katika uwanja wa Nyayo.

Bao hilo moja na la ushindi katika mtanange huo lilifungwa na Maxwell Otieno kunako dakika ya tano na kuwafanya chui hao wanaoongozwa na mkufunzi Patrick Aussems kuvuna ushindi huo.

Matokeo ya mechi hiyo sasa yanaifanya Afc Leopards kupanda hadi nafasi ya 7 na alama 21 huku Vihiga Bullets ikishuka hadi nafasi ya 17 na alama 4 pekee.

Akizungumzia matokeo ya mechi hiyo mkufunzi wa Vihiga Bullets George Owoko amesema kwamba ukata wa kifedha na ukosefu wa udhamini ndio donda sugu katika klabu hiyo jambo ambalo linakosesha motisha vijana wake.

Baada ya mechi ya jana Vihiga Bullets walikuwa wamekwama jijini Nairobi kutokana na ukosefu wa hela za usafiri wa kurejea Nyumbani. Mbunge wa Makadara George Aladwa jana alilazimika kujitolea na kuwapa msaada wa tikiti elfi 35000 za kuwasaidia kurejea nyumbani katika kaunti ya Vihiga.