Wazazi wa wanafunzi wanaopaswa kujiunga na shule za upili mwaka huu wa 2023 wametakiwa kutochapisha fomu zilizo na taarifa kuhusiana na shule wanazopaswa kujiunga nazo, iwapo hawana uwezo ama hawajaridhishwa na taasisi hizo na badala yake waziwasilishe katika afisi za elimu kwenye maeneo yao.
Haya ni kwa mujibu wa katibu wa muungano wa walimu wa KNUT tawi la Mombasa, Dan Aloo ambaye amesema huenda wazazi wengi wakakosa kuwa na uwezo wa kumudu karo za baadhi ya shule ambazo, watoto wao wanapaswa kujiunga nazo.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na mwanahabari wetu, katibu huyo amewasisitizia wazazi kutoa sababu mwafaka za wao kutoridhishwa na shule hizo, kabla ya wao kuafikia uamuzi wa kutafuta shule mbadala.
Wakati huohuo Aloo amesema yapo makosa mengi ambayo hufanyika katika shughuli nzima ya kuwachagulia wanafunzi shule za upili, ambazo wanapaswa kujiunga nazo, jambo ambalo amesema ni sharti wizara ya elimu izingatie kurekebisha na hata kuboresha.

