UKOSEFU WA MAJI SAFI KWA MUDA MREFU WAZIDI KUWAATHIRI WENYEJI WA KINANGO

Wakaazi wa Kinango kaunti ya Kwale wamelalamikia ukosefu wa maji safi kwa muda wa miezi mitano mtawalia.

Wakaazi hao wakiongozwa na Hamisi Mzungu wamewakosoa wasimamizi wa bodi ya usambazaji maji pwani sambamba na kampuni ya usambazaji maji kaunti hiyo ya Kwale Kwawasco.

Wamesema wanapaswa kutafutiwa mwafaka wa haraka wakieleza kusikitishwa na swala kuwa chemchemi ya maji ya Marere iliyopo katika eneo hilo imekuwa ikitumika kusambaza maji hadi kaunti ya Mombasa ilhali eneo lao halina maji.

Wamesema kuwa ukosefu huo wa maji umeathiri pia utoaji wa huduma za afya mbali na shughuli nyenginezo za kuimarisha eneo hilo kiuchumi huku wakilalamikia kuwa uhaba huo wa maji pia unaathiri pakubwa mahusiano ya ndoa kwa wanajamii.