HARAKATI ZA KUWASAKA WANAFUNZI WATAKAODINDA KUREJEA SHULENI WIKI IJAYO KUANZISHWA MALINDI

Naibu chifu wa Shella mjini Malindi kaunti ya Kilifi, Nicodemus Mwayele amesema kuwa wanalenga kuanzisha msako dhidi ya wanafunzi watakaokosa kurudi shule juma lijalo.

Kwa mujibu wa Mwayele, tayari wamekamilisha vikao vya kuweka mikakati ya jinsi watakavyotekeleza shughuli hiyo kwa ushirikiano na wazee wa mitaa, waliokatika maeneo mbalimbali ya eneo bunge la Malindi.

Akizungumza na wanahabari ameeleza kuwa hawajapokea kisa chochote cha mwanafunzi wa kike, aliyepachikwa ujauzito katika likizo ambayo kwa sasa inaendelea kutamatika.

Aidha, Mwayele amesema kuwa wazazi watakaokosa kuwapeleka wanao shuleni watakabiliwa kwa mujibu wa sheria huku akitaja jamii eneo la Kajajini hapa mjini Malindi, kuwa na idadi kubwa ya watoto ambao hawapelekwi shuleni.