MBUNGE WA MALINDI AMINA MNYAZI ASEMA KUNA HAJA YA WAKULIMA WA KAKUYUNI KUWEZESHWA

Ipo haja ya wakulima katika wadi ya Kakuyuni eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi kuwezeshwa, ili kuhakikisha wanapata mazao bora katika mashamba yao.

Ni kauli ya mbunge wa Malindi kaunti ya Kilifi, Amina Mnyazi ambaye amesema matatizo mengi katika eneo hilo, yatapata suluhu iwapo wananchi watakuwa na vyakula vya kutosha kutokana na kilimo wanachofanya.

Akizungumza na wananchi katika eneo hilo, ameahidi kulipa kipaumbele zaidi suala la Elimu na kilimo bora katika wadi hiyo, kwani ni uti wa mgongo wa wanajamii wengi walioko katika wadi hiyo.

Wakati huohuo amempongeza mwakilishi wa wadi wa  eneo la Kakuyuni  Morris Hinzano, kwa kuwa mwakilishi wa wadi wa kwanza katika eneo bunge la Malindi, kuwasilisha majina kamili ya wanafunzi wote wenye uhitaji wa karo katika wadi yake, kwa afisi ya mbunge huyo, jambo ambalo amesema litasaidia kuimarisha mipango ya ugavi wa fedha za basari.