GAVANA ABDULSWAMAD APANIA KUFANYA UKAGUZI KUBAINI WAFANYIKAZI HEWA

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir anapanga kufanya ukaguzi kubaini wafanyikazi hewa waliokuwepo tangu serikali ya kaunti iliyopita chini ya uongozi wa gavana mstaafu Ali Hassan Joho.
Akizungumza afisini mwake Abdulswamad amesema tayari ameiandikia barua tume ya huduma za umma kuishurutisha kufanya ukaguzi kuhusiana na Suala la wafanyikazi hewa.
Kauli yake inajiri baada ya kuenea kwa ripoti kuwa takribani shilingi bilioni 3 zilitumika kulipa wafanyikazi hewa katika serikali ya kaunti iliyopita.
Abdulswamad ameeleza kuwa katika harakati za kutaka kubaini ukweli wa ripoti hiyo aliarifiwa kuwa ilikuwa ni ripoti ya tangu mwaka wa 2013 wakati ambapo serikali mpya ya kaunti ilifanya ukaguzi wake baada ya kuchukua uongozi kutoka kwa serikali iliyokuwepo ya Manispaa wala si ripoti ya hivi karibuni.