ZAIDI YA FAMILIA 4,000 TAITA TAVETA KUNUFAIKA NA CHAKULA CHA MSAADA

Mshirikishi wa shirika la msalaba mwekundu kanda ya pwani Hassan Musa amesema zaidi ya familia elu 4 kaunti ya Taita Taveta zinatarajiwa kunufaika na chakula cha msaada kutoka kwa wafadhili mbalimbali kupitia shirika hilo.
Akizungumza mjini Voi, Hassan amesema shirika la msalaba mwekundu linashirikiana na serikali ya kaunti ya Taita Taveta na ya kitaifa ili kutambua familia ambazo zimeathirika zaidi na baa la njaa.
Amesema watahakikisha pia shule ambazo ziliathirika na baa la njaa zinanufaika na chakula hicho cha msaada ili kuwawezesha wanafunzi kuendeleza masomo yao bila changamoto zozote.
Vilevile, ametoa wito kwa serikali kuu na zile za kaunti kushirikiana ili kuweka mikakati ambayo itakabiliana na kiangazi nchini katika siku za usoni.