Imebainika kuwa idadi ya wakaazi wa kaunti ya Kilifi waliochanjwa dhidi ya virusi vya Corona kaunti ya Kilifi ni ndogo mno ikilinganishwa na matarajio ya wizara ya afya kuhusiana na utoaji wa chanjo hiyo.
Shirika la msalaba mwekundu limesema ni asilimia 19 pekee ya wakaazi wa kaunti ya Kilifi waliochanjwa dhidi ya virusi hivyo hali inayohatarisha maisha ya wenyeji hao.
Kufuatia hilo, naibu katibu mkuu wa shirika hilo la msalaba mwekundu, Annette Msabeni amesisitiza haja ya jamii kuendelea kuhamasishwa kuhusiana na umuhimu wa kuchanjwa dhidi ya virusi vya Corona.
Msabeni amesema tayari shirika hilo linashirikiana na AMREF pamoja na Africa CDC kutoa hamasa kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa kuchanjwa.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo wa uhamasishaji wa chanjo ya virusi vya korona, Msabene amesema mradi huo umeratibiwa kufanyika katika kaunti nane, ya Kilifi ikiwa miongoni mwao.
Ni kauli ilioungwa mkono na mratibu wa mradi huo, Charles Ibeneme ambaye amesema maambukizi ya msambao wa virusi vya Corona yatadhibitiwa iwapo jamii itaendelea kuchanjwa na kupongeza ushirikiano baina ya mashirika hayo katika juhudi za kupambana na virusi vya Corona nchini.
IDADI YA WALIOCHANJWA CHANJO YA COVID -19 KAUNTI YA KILIFI IKO CHINI

