HIMIZO LAZIDI KUTOLEWA KWA WATU WENYE UATILIFI KAUNTI YA KILIFI KUJISAJILI

Mwakilishi wa watu wenye uatilifu kaunti ya Kilifi, Tima Abu amesisitiza haja ya watu wenye uwezo maalumu kusajiliwa ili kurahisisa zoezi la kuwapatia misaada ya msingi watu hao wenye uwezo maalum.
Akizungumza katika kikao cha kutoa hamasa kwa jamii kuhusiana na watu wenye uatilifu, kikao kilichoandaliwa na shirika la Women challenged to challenge, Tima amesema kuwa baada ya kuwasilisha lalama zao kwa mbunge wa Malindi, Amina Laura Mnyazi, changamoto zinazokumba watu wanaoishi na ulemavu hapa Malindi haziwezi kutatuliwa iwapo hawajajulikana kiidadi.
Tima amesema ili watu hao wanaoishi na ulemavu wanufaike pamoja na jamaa zao ni sharti wajisajili kwenye baraza maalum ili idadi yao ikajulikane kabla ya kuwekewa mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazowakumba.
Aidha amesema kuwa watu wanaoishi na ulemavu wamekuwa wakinyanyaswa na jamii hasa katika kutoa nafasi za ajira.
Tima amesema kuwa watu wanaoishi na ulemavu ambao pia wanaugua kifafa wanapitia ugumu kupata huduma za afya zinazofungamana na ugonjwa huo ikizingatiwa kwamba hospitali ya rufaa ya Malindi haina daktari maalum anayeshughulikia ugonjwa huo.
Wakati uo huo Tima amesema kuwa watu wanaoishi na ulemavu wanapaswa kuimarishwa kiuchumi ili kuhakikisha kuwa wanaweza kujimudu.