GAVANA MUNG’ARO ATEULIWA KUWA MWENYEKITI WA JUMUIYA YA KAUNTI ZA PWANI

Kuna haja ya magavana ukanda wa pwani kudumisha ushirikiano miongoni mwao kwa minajili ya kuimarisha hadhi ya eneo hili la pwani.
Haya ni kwa mujibu wa gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Maitha Mung’aro ambaye amesema ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa viongozi waliotangulia katika ukanda wa pwani umechochea eneo la pwani kusalia nyuma kimaendeleo.
Akizungumza kwenye kaunti ya Mombasa baada ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa jumuiya ya kaunti za pwani, Mung’aro amesema ni sharti magavana wa pwani waweke kando tofauti zao za kisiasa na badala yake washirikiane ili wawavutie wawekezaji katika ukanda huu wa pwani.
Ni kauli iliyoungwa mkono na mkurugenzi mkuu wa jumuiya hiyo ya kaunti za pwani, Emmanuel Nzai akisema ni jukumu la magavana hao kupigania haki za wakaazi wao na wapwani kwa jumla sawia na kuimarisha sekta ya uchumi wa pwani.