Maafisa watatu waliokuwa wakifanya kazi katika serikali ya kaunti ya Tana River, wamekanusha mashtaka dhidi yao kuhusiana na utumizi mbaya wa afisi za umma katika kaunti hiyo, kwenye mahakama ya Malindi kaunti ya Kilifi.
Watatu hao ambao ni Mohamed Muhammad Guracho, afisa mkuu wa idara ya maji kaunti ya Tana River, Salim Juma Makorani ambaye ni meneja wa idara ya maji ya TAWASCO na Gwiyo Makugo Madubi mkurugenzi wa idara hiyo, wamehusishwa na ufujaji wa shilingi milioni 3.5, zilizokuwa zimeratibiwa kurekebisha visima vya maji kaunti hiyo kandarasi iliyokuwa imekabidhiwa kampuni ya M/S Shirtliff eneo la Mororo Madogo.
Kulingana na mahakama hiyo, watatu hao wametajwa kutekeleza mashtaka hayo mnamo februari mwaka 2016, walipokuwa wakihudumu kama maafisa wa kaunti hiyo.
Aidha, hakimu mkuu wa mahakama ya Malindi Bi Elizabeth Usui, amewaachilia watatu hao kwa dhamana ya shilingi milioni 1 au shilingi laki tano pesa taslimu kwa kila mmoja.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 6 mwezi wa 10 mwaka huu wa 2022, ambapo tarehe ya kusikizwa kwa kesi pia hiyo itatolewa siku iyo hiyo.

