Idadi kubwa ya wenyeji wa kaunti ya Kilifi wanadaiwa kuwa na matatizo ya macho, hali ambayo inadaiwa kuchangiwa na maradhi ya kisukari mwilini mwao.
Haya ni kwa mujibu wa msimamizi wa hospitali ya Kibinafsi ya Mephi mjini Kilifi kaunti ya Kilifi Rita Mukhongo, ambaye amesema wengi wa wakaazi hawana ufahamu wa kuwa wanaugua maradhi ya kisukari, kwani hawajawahi kufanyiwa vipimo vya ugonjwa huo
Akizungumza katika eneo la Matsangoni wakati wa zoezi la matitabu ya bure lililofadhiliwa na hospitali hiyo, Rita amesema kuwa ipo haja ya wale wanaokumbwa na matatizo ya macho, kufanyiwa vipimo vya kisukari ili kupata matibabu ya haraka kabla ya maradhi hayo kuathiri sehemu zingine za mwili.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wakiongozwa na Emmanuel Kazungu na Priscila Mapenzi, wamepongeza hatua ya kituo hicho cha afya kutekeleza zoezi hilo kwa wananchi na kusema kuwa ipo haja ya kuwepo kwa shughuli hizo kwa wingi, kwani idadi kubwa ya wananchi wameendelea kuugua majumbani kutokana na hatua ya wao, kutokuwa na fedha za kugharamikia matibabu hayo hospitalini.

