Mbunge wa Malindi kaunti ya Kilifi, Amina Mnyazi ameitaka wizara ya uchukuzi, kupitia kamati yake kwenye bunge la kitaifa, kuweka wazi mikakati iliyoko, katika kupunguza visa vya ajali za ndege kwa wanafunzi wanao somea urubani.
Kulingana na Mnyazi, licha ya kuwepo kwa uchunguzi kuhusiana na chanzo cha ajili ya ndege, iliyosababisha vifo vya watu wawili eneo la Kwa Chocha hapa mjini Malindi, bado kamati hiyo haijaweka wazi mikakati iliyopo, kudhibiti ajali za ndege.
Akizungumza katika kikao kwenye bunge la kitaifa, kiongozi huyo amesisitiza kuwa mikakati hiyo, itasaidia kuondoa wasiwasi kwa wasafiri na hata wananchi wanaoishi karibu na uwanja wa ndege wa Malindi, kuhusiana na kushuhudiwa kwa kisa sawia na hicho katika siku zijazo.
Mbunge huyo amesema kuna haja ya kamati hiyo kutoa taarifa mwafaka itakayo angazia chanzo cha ajali hiyo, ambayo pia itaelezea mikakati ya serikali, kuhusiana na kulipa fidia familia za waathiriwa wa ajili hizo.

