WENYEJI WA KAMALE WANAENDELEA KUKABILIWA NA KIANGAZI NA BAA LA NJAA

Wenyeji wengi katika eneo la Kamale huko Hadu kaunti ndogo ya Magarini kaunti ya Kilifi wanaendelea kuathirika na baa la njaa na ukame kutokana na kiangazi ambacho kinazidi kushuhudiwa katika eneo hilo.
Mmoja wa wenyeji hao, Kahindi Ndoro anasema kwa kipindi cha miaka minne hakujashuhudiwa mvua katika eneo hilo hali ambayo imeathiri shughuli za kilimo maeneo hayo.
Amesema tegemeo lao kuu ni msaada kutoka kwa wahisani mbalimbali na bado wanaendelea kuathirika kwani chakula cha msaada wanachopata hakiwezi kuwatosheleza.
Aidha, amesema kutoka na kiangazi na baa la Njaa imekuwa vigumu kwa watoto wao kuhudhuria masomo shuleni.
Kwa upande wake Justine furaha Karisa ambaye ni Naibu chifu wa eneo hilo la Kamale amesema kupitia kikundi cha kijamii cha “Nahumanyane Ahenzwi” wameweza kuwapa wenyeji hao chakula cha msaada na kutoa wito kwa mashirika na wahisani mbalimbali kujitokeza kwa wingi ili kuwanusuru wenyeji hao.