WAPWANI WAPONGEZA UTEUZI WA FIKIRINI JACOBS KWENYE WADHIFA WA KATIBU KATIKA SERIKALI KUU.

Gavana wa kaunti ya Kilifi amejiunga na wakaazi wengine wa kaunti hii, katika kumpongeza kiongozi wa vijana kwenye chama cha ODM, kaunti ya Kilifi, Fikirini Jacobs kwa kuteuliwa kuwa katibu wa idara ya vijana na michezo kwenye serikali kuu.

Akizungumza na waandishi wa habari, gavana Mung’aro amempongeza Fikirini pamoja na Profesa Abdulrazak Shaukat, mkaazi wa eneo la Mariakani hapa kaunti ya Kilifi, kwa uteuzi wao huku akisema kuwa hatua hiyo, itawapatia vijana wa Gen Z hakikisho la serikali ya kitaifa, kuzingatia matakwa yao.

Mung’aro amewatakia wawaili hao kila la kheri, katika zoezi linalo wasubiri la kupigwa msasa na kamati ya uteuzi kwenye bunge la kitaifa huku akielezea kuwa na imani, ya wawili hao kuidhinishwa na viongozi wa bunge hilo.

Kwa upande wao baadhi ya wakaazi wa eneo bunge hili la Malindi kaunti ya Kilifi, wakiongozwa na Samuel Safari na Edwin Thoya, wamesema kuwa hatua hiyo imewatia moyo wafuasi wa chama cha ODM, kuendelea kuunga mkono muungano kati ya Rais William Ruto na Raila Odinga.

Aidha, baadhi ya wananchi wameibua hisia kinzani na kudai kuwa, hatua hiyo ni njama ya rais William Ruto, kuwashawishi viongozi wa ODM eneo la Pwani kujiunga na chama cha UDA.