Naibu wa Rais Profesa Kithure Kindiki amewataka viongozi wa kisiasa mashinani, kuweka kando tofauti zao za kisiasa na badala yake, kuendeleza mazungumzo ya kuboresha maendeleo ya jamii.
Kindiki ambaye alikuwa akizungumza kwenye kikao na viongozi wa kaunti ya Meru, katika makaazi yake jijini Nairobi, amewaonya wanasiasa nchini dhidi ya kuchukiana kwa misingi ya siasa, baada yao kukosa kuchaguliwa kwenye nafasi mbali mbali za uongozi.
Naibu huyo wa rais, amesema kuwa iwapo viongozi wa kisiasa wataendeleza malumbano kati yao, wananchi walio wachagua wataendelea kukabiliwa na changamoto mbali mbali mashinani.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa kaunti hiyo na Kenya kwa jumla, kushirikiana ili kuboresha shughuli za maendeleo kwenye jamii.

