WAHANDISI NCHINI KENYA WAPINGA SUALA LA SOMO LA HISABATI KUWA LA HIARI KWA WANAFUNZI WA MTAALA CBC NCHINI KENYA.

Taasisi ya Wahandisi nchini IEK (Institution of Engineers of Kenya), imepinga hatua ya Wizara ya Elimu, kutaka somo la hisabati kuwa la hiari kwa wanafunzi.

Taasisi hiyo ya wahandisi IEK, imesema kuwa Hisabati ni somo muhimu, ambapo kila mwanafunzi, wanapaswa kulazimishwa kulifanya kama ilivyo kwa sasa.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Rais wa IEK, Shammah Kiteme, wizara ya Elimu inapaswa kurejesha kigezo cha Hisabati kwa wanafunzi wote wanaopania kujiunga na vyuo vikuu nchini.

IEK imesema, hisabati ni somo kuu kwa taaluma nyingi, ikiwemo viwanda, kawi, miundo msingi na teknolojia ya habari na mawasiliano, na kamwe halipaswi kuwa la hiari kwa wanafunzi.

Badala yake, IEK imevitaka vyuo vyote vya kiufundi na vyuo vikuu, kuweka kigezo cha somo la hisabati na sayansi kwa wanafunzi wote, wanaotaka kusomea taaluma za sayansi na zile za kiufundi.

Wizara ya elimu wiki iliyopita, ilitangaza kuwa wanafunzi wa gredi ya tisa, hawatalazimishwa kusoma Hisabati, bali watachagua masomo kulingana na taaluma wanazopania kujiunga nazo.