UTALII PWANI WADAIWA KUCHANGIA ONGEZEKO LA VISA VYA DHULMA ZA KIJINSIA.

Washikadau mbali mbali katika mashirika ya kijamii kaunti ya Kilifi pamoja na wanasheria, wamekongamana katika kaunti ya Kilifi ili kujadili kuhusiana na mikakati ya kukabiliana na ongezeko la visa vya dhulma za kingono eneo la Pwani.

Kulingana na wadau hao ni kuwa kaunti ya Kilifi, Kwale na Mombasa ni mojawapo ya kaunti za Pwani ambazo zimekuwa zikiongoza kwa idadi ya visa vya dhumla hizo, suala ambalo wanadai kuchagiwa na shughuli za kitalii zinazo endeshwa katika kaunti hii.

Akifungua rasmi kongamano hilo la siku mbili, Yvonne Oyeke wa shirika la Equality Now amesema kuwa lengo kuu la kongamono hilo ni kuangazia baadhi ya sheria, zinazotumika kuwakabili wale wanaotekeleza visa hivyo, ili kuhakikisha kuwa waathiriwa wapata haki.

Kwa upande wake Paul Adhoch, mkurugenzi mkuu wa shirika la Trace Kenya amesema kuwa wanatarajia kuwa huenda visa hivyo, vikapata suluhu la kudumu hasa vile vinavyo husisha watoto waliochini ya umri wa miaka 18, kutokana na hatua ya aliyekuwa mbunge wa Malindi Bi Aisha Jumwa, kuteuliwa katika wadhifa wa Waziri wa Masuala Jinsia humu nchini.