TANI 54,000 ZA NGANO ZAWASILI BANDARINI MOMBASA

Shehena ya ngano kutoka nchi ya Ukraine iliwasili jana katika bandari ya Mombasa.
Balozi wa Ukraine nchini Andrii Pravednyk amesema kuwa tani hizo 54,000 zitasaidia taifa kukabiliana na uhaba wa nafaka na kumaliza mfumuko wa bei.
Amesema taifa la Kenya limekuwa likikabiliwa na uhaba wa ngano na tani hizo zitaifaidi nchi hii, mikakati zaidi inapoendelea kuwekwa kuboresha ukuzaji wa ngano nchini ili kudhibiti uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka mataifa mengine.
Balozi Andrii anasema ingawa wamefaulu kusafirisha nafaka hiyo chini ya mkataba wa kuruhusu meli kusafirisha chakula duniani, ghala na mashamba ya chakula Ukraine yameharibiwa na mabomu ya Russia.
Vilevile, amesema ukosefu wa mbegu bora za kilimo umechangia kwa mazao duni kushuhudiwa nchini Kenya.
Meli zingine mbili zinatarajiwa kuwasili Mombasa hivi karibuni zikiwa na shehena ya tani milioni 78 ya ngano na Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa zaidi ya watu milioni 4 nchini Kenya wanakabiliwa na ukosefu wa chakula na inatarajiwa kwamba chakula kilichopokelewa leo kutoka Ukraine kitasaidia kupunguza bei ya chakula hasa ngano.