Serikali ingali inamsaka afisa wa polisi raia wa Kenya, aliyetoweka nchini Haiti, baada ya shambulizi lililotekelezwa na wahalifu wa nchi hiyo, dhidi ya maafisa wa Kenya, wanaoendeleza oparesheni ya usalama nchini humo.
Inspekta generali wa polisi Douglas Kanja, anasema kufikia sasa bado afisa huyo hajulikani aliko, licha ya taarifa ya kuhusiana na kifo chake kusambaa mitandaoni.
Kanja amesema kuwa wanaendeleza oparesheni ya kumsaka afisa huyo, katika taifa hilo la Haiti huku akiahidi familia yake kuwa mpendwa wao atapatikana na kurejea nyumbani.
Hata hivyo Kanja amesema kuwa maafisa wa polisi, ambao wamekuwa wakijeruhiwa kwenye oparesheni hiyo, wanapokea matibabu bora inje na ndani ya taifa hilo.
Haya yanajiri huku maafisa wengine wawili wa Kenya, walioko nchini Haiti wakijeruhiwa vibaya kufuatia mapigano na magenge ya kihalifu nchini humo.
Msemaji wa kikosi Cha Usalama wa kimataifa nchini Jack Ombaka, anasema maafisa hao waliojeruhiwa wanapokea matibabu katika jamhuri ya Dominika.

