Rais William Ruto amewasuta baadhi ya viongozi na wakenya wanaopinga mfumo wa bima ya matibabu wa SHA huku akiwataja kuwa wafisadi waliochangia katika wizi wa fedha za umma, katika bima ya awali ya NHIF.
Rais Ruto amepuuziluia mbali vilio vya wakenya, kuhusiana na changamoto za bima hiyo huku akisema serikali ya kitaifa, haita legeza msimamo wake wa kurejea kwenye bima hiyo ya awali ya NHIF.
Akizungumza katika mazishi ya mbunge wa Malava kaunti ya Kakamega, Moses Malulu, ambaye aliaga dunia wiki chache zilizopita, baada ya kuugua kwa mda, rais amepigia debe mfumo wa SHA, akisema kuwa umeziba mianya ya ufisadi katika sekta ya afya.
Kauli yake imeungwa mkono na spika wa bunge la kitaifa Moses Masika Wetangula, ambaye amewataka wakenya kujisajili kwenye bima hiyo mpya.
Aidha, kiongozi wa wengi kwenye bunge la kitaifa Kimani Ichungwa, ameelezea kuwepo kwa manufaa ya huduma za bure kwenye mpango huo huku mwenzake wa bunge la seneti Aron Cheriyot, akizomewa na waombolezaji baada ya kudai kuwa serikali za kaunti, tayari zimelipwa fedha za wagojwa watakaotibiwa hadi mwaka ujao Januari.

