Nyota Wa Zamani Wa Harambee Stars Amkingia Kifua Cristiano Ronaldo

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Harambee Stars, Bonface Ambani amemtetea nyota wa klabu ya Manchester United, Cristiano Ronaldo baada ya klabu hiyo kutangaza kuwa hatashiriki mechi yao ya ligi dhidi ya Chelsea.

Ambani ambaye aliwahi kuichezea klabu ya Yanga SC ya Tanzania msimu wa kati ya mwaka 2009 na 2010 , alitumia mitandao ya kijamii akisema kuwa mameneja wengi wa klabu hawajui jinsi ya ‘kuwashughulikia’ wachezaji wao.

“Suala la Cr7 huko Utd ni mjadala mzito. Nitakuambia bure. Asilimia 90 ya makocha kote ulimwenguni hawajui jinsi ya kushughulikia nyota katika timu zao,” sehemu ya chapisho la mtandao wa kijamii la Ambani ilisoma.

Gwiji huyo wa soka aliendelea kusema kuwa hiyo ni sababu mojawapo inayowafanya wachezaji wengi nchini Kenya kutundika daluga zao wakiwa wachanga.

“Naweza kuelezea yanayomkuta CR7 katika klabu ya Utd. Waulize wachezaji wa haiba ya juu jinsi walivyostaafu kutoka kwa vilabu hivi. Najua utakuja na nadharia zote, lakini nabaki thabiti kukuambia ukweli.

“Inferiority Complex huwa inaingia. Anyway, inategemea na unavyoiona, lakini la msingi… Usiniambie etiii Cr7 time imekwisha. Hao wachezaji wakubwa sio watu wa Ku train daily kama Stephen Mukangai … nani ni miaka 20 tu.
Nimeenda Shiseno,” Ambani alimalizia maelezo yake kwa ucheshi.

Cr7 issue at Utd is a serious discussion. I will tell you for free. 90% of coaches all over the world don't know how to…

Posted by Bonface Ambani on Thursday, October 20, 2022

Ambani aliwahi kuitumikia klabu inayoshiriki ligi kuu nchini, Tusker FC, kati ya 2004 na 2006 akifunga mabao 27 katika mechi 26 alizocheza. Baadaye alisaini mkataba na klabu ya soka ya India yenye mafanikio mengi, East Bengal.

Aliwasaidia East Bengal kumaliza nafasi ya saba msimu wa 2006-2007.

Msimu wa awali East Bengal walikuwa wamemaliza katika nafasi ya tisa kwenye jedwali la ligi. Klabu yake ya mwisho kuichezea ni Yanga SC ya Tanzania.

Erik ten Hag aliamua kumtupilia Ronaldo nje ya kikosi cha safari ya Stamford Bridge baada ya kuondoka uwanjani mapema kufuatia ushindi wa United wa 2-0 dhidi ya Spurs Jumatano usiku.

Mreno huyo hatashiriki katika mazoezi ya kikosi cha kwanza kwa wiki nzima na hatakuwa sehemu ya watakaosafiri kumenya na Chelsea, badala yake atafanya mazoezi peke yake Carrington.

Ronaldo aliindoka uwanjani zikiwa zimesalia sekunde 30 za muda wa kawaida, pamoja na dakika nne za nyongeza.