MCHUNGAJI PAUL MACKENZIE ATIWA MBARONI

Maafisa wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai, DCI mjini Malindi kaunti ya Kilifi wamemtia mbaroni mchungaji Paul Mackenzie wa kanisa la good news international, ambaye anadaiwa kuwapotosha kiimani wakaazi wa eneo la Shakahola kwa kuwataka kutowapa watoto wao chakula jambo ambalo limechangia kwa idadi kubwa ya watoto kuaga dunia.
Kulingana na baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wakiongozwa na Francis Wanje, anadai wajukuu wake wawili waliaga dunia baada ya wazazi wao kupata mafunzo ambayo yanaposha kiimani kutoka kwa mchungaji huyo, ambaye aliwashurutisha watoto hao kuingia katika mfungo hadi pale watakapoaga dunia.
Akizungumza na wanahabari wakati wa oparesheni ya kukamatwa kwa mchungaji huyo, Wanje amesema mchungaji huyo amekuwa akidai yapo majanga ambayo huenda yakashuhudiwa katika siku za usoni na hivyo basi ni vyema kwa watoto hao kuaga dunia ili waurithi ufalme wa mbinuguni.
Vilevile, ameibua madai kuwa takribani watoto 30 wamezikwa baada ya kuaga dunia katika hali hiyo, suala ambalo bado maafisa wa polisi hawajathibitisha.
Taarifa za kukamatwa kwa Paul Mackenzie zimethibitishwa na Kamanda wa polisi mjini Malindi kaunti ya Kilifi, John Kemboi ambaye ameahidi kutoa taarifa kamili kuhusiana na idadi ya watoto walioaga dunia pamoja na taarifa zingine kuhusiana na tukio hilo leo Alhamisi.