Huduma za afya katika kaunti tatu za pwani zinatarajiwa kuimarika katika siku za usoni, baada ya mamlaka ya maendeleo eneo la pwani CDA, kuzindua ujenzi wa vyumba vya wagonjwa, wanaohitaji huduma maalum katika hospitali ya Malindi kaunti ya Kilifi.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, mwenyekiti wa mamlaka hiyo Mzee Mwinyi Mzee, anasema mradi huo unaotekelezwa na serikali ya Italia, kupitia mamlaka hiyo, utasaidia wagonjwa kutoka kaunti za Lamu, Tana River na Kilifi.
Mwinyi amesema Kwa muda Sasa, wangojwa wanaohitaji huduma hizo wamelazimika kusafiri hadi kaunti ya Mombasa, hatua ambayo amesema huwalazimu wagonjwa kugharamika zaidi.
Naye kaimu mkurugenzi wa mamlaka hiyo Pamela Maghema, amesema ujenzi wa mradi huo pamoja na vifaa hitajika, baada ya kukamilika kwa ujenzi wake utagharibu zaidi ya shilingi milioni mia moja.
Aidha, waziri wa afya katika kaunti ya Kilifi, Peter Mwarogo amesema mradi huo unatatekelezwa katika kipindi Cha miezi minane na utapiga jeki sekta ya afya kaunti ya Kilifi.
Mamlaka hiyo tayari ilikamilisha ujenzi wa vyumba vya wagonjwa mahututi katika hospitali hiyo ya Malindi.

