MAHAKAMA YA HARAMISHA AGIZO LA SERIKALI KUHUSIANA NA MALIPO YA KARO KUPITIA MTANDAO WA ECITIZEN.

Serikali ya kitaifa imepata pigo baada ya Mahakama Kuu, kuamua kuwa agizo la kuwataka wazazi kulipa karo kupitia mfumo wa eCitizen ni kinyume cha sheria.

Mnamo Januari 2024, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Elimu Belio Kipsang, kupitia waraka aliagiza malipo yote ya karo ya shule za umma, yafanywe kwenye mfumo huo.

Jaji Chacha Mwita, akitoa uamuzi wake leo Jumanne, alipiga marufuku serikali kutekeleza agizo hilo, akisema kwamba umma haukushirikishwa  kabla ya utekelezwaji wake.

Mwita Pia, alibainisha kuwa ada inayotozwa ya Ksh.50, ili kupata huduma hiyo haina msingi wa kisheria.

Mahakama pia imetilia shaka uadilifu na uwazi wa jukwaa la eCitizen, ikibainisha kuwa haijulikani ni nani anayekusanya pesa hizo na zinawekwa wapi.

Jaji Mwita amesisitiza kuwatoza wazazi ada ya ziada ni sawa na kutozwa ushuru mara mbili.

Kesi hiyo iliwasilishwa na Daktari Magare Gikenyi, mkaazi wa Nakuru, ambaye alidai kuwa hakuna sheria au mfumo unaoelekeza jinsi pesa hizo zinavyotumika au kurejeshwa kwa watumiaji wa mwisho.

Pia alitilia shaka sababu za ada ya ununuzi ya Ksh.50 na kusema kuwa agizo hilo linaweza kuwaathiri wazazi wanaolipa karo kama vile ya  mahindi au maharagwe.