KOCHA WA ZAMANI WA MAN CITY AAGA DUNIA

MKUFUNZI wa zamani wa klabu ya Manchester City, Sven-Göran Eriksson, raia wa Sweden, aaga dunia akiwa na umri wa miaka 76.

Hadi anaaga dunia, Sven alikuwa amenoa vilabu vya soka 13 na timu 3 za taifa ikiwa ni pamoja na timu ya taifa ya Uingereza, THE THREE LIONS, kati ya mwaka 2001 hadi 2006.

Vilabu maarufu alivyowahi kuvipatisha makali ni pamoja na Manchester City, Leicester City, Roma, Benfica, Sampdoria na Lazio.

Ivory Coast au Côte d’Ivoire kama inavyotambulika na FIFA ni timu ya pekee kutoka Afrika kuwahi kunolewa na Sven. Sven aliwasaidia NDOVU hao kufuzu kucheza kombe la dunia 2010.

Wakati anateuliwa kuwa meneja wa Uingereza Sven Goran Eriksson aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama meneja wa kwanza wa kigeni nchini humo kukinoa kikosi cha Uingereza.

Sven alikuwa maarufu sana nchini Uingereza, hata ulihitaji tu kutaja jina lake la kwanza na kila mtu – awe ni shabiki wa soka au la – alijua unazungumza nani.

“Kwa niaba ya jumuiya ya soka la Ulaya, kila mtu UEFA amehuzunishwa sana na kifo cha Sven Göran Eriksson,” UEFA imesema katika mtandao wa X zamani ukijulikana kama Twitter.

“Akiwa mpendwa kwenye mchezo huu wa soka, Sven alikuwa mshindi wa Kombe la UEFA kama kocha wa IFK Göteborg mnamo 1982 kabla ya kuiongoza Lazio kwenye ushindi wa Kombe la UEFA mnamo 1999.”

Meneja wa timu ya Uingereza Sven-Goran Eriksson na Wayne Rooney wakiwa katika mazoezi ya Kombe la Dunia 2006

 

Klabu ya Liverpool na Fiorentina ni baadhi ya vilabu ambavyo tayari vimetoa rambirambi kuomboleza kifo cha nguli huyo wa soka.

“Pumzika kwa amani, Sven-Göran Eriksson. Mawazo ya kila mtu kwenye klabu yako pamoja na familia na marafiki wa Sven katika wakati huu wa huzuni sana,” Liverpool imeandika kwenye mtandao wa X.

Man City wameandika kwenye X wakisema, “Tungependa kutoa rambirambi zetu za dhati kwa familia na marafiki wa Sven-Goran Eriksson, ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 76. Pumzika kwa amani, Sven.”

BURIANI SVEN.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *