KALONZO MUSYOKA AKOSOA UTENDAKAZI WA SERIKALI YA KENYA KWANZA.

Kinara wa chama Wiper, Kalonzo Musyoka amezidi kuikosoa serikali ya Kenya kwanza, kwa madai kwamba imeshindwa kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi, wakati wa siasa za uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2022.

Akizungumza mjini Malindi kaunti ya Kilifi, wakati wa ufunguzi wa afisi za chama cha Wiper, Kalonzo ameitaja bima mpya ya afya ya SHA, kutokuwa na manufaa kwa wananchi, kwani wengi wao wameendelea kutabika wakati wakitafuta huduma za matibabu.

Kalonzo aidha amesema viongozi wa upinzani, hawatakubali udanganyifu wa aina yeyote, wakati wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027 huku akiwataka wananchi, kujitokeza na kupeleka nyumbani viongozi wasiowajibika.

Aidha, kiongozi huyo amebainisha kuwa wanalenga kuandaa kikao na wabunge wa upinzani, ili kutoa msimamo wao baada ya mahakama kutoa uamuzi, kwamba viongozi wengi katika bunge la kitaifa, ni wale wa Azimio la Umoja One Kenya.