Wakfu wa benki ya I&M, unapania kupanda miti milioni kumi katika maeneo mbali mbali ya taifa hili, kufikia mwaka ujao wa 2026.
Haya ni kwa mujibu wa afisa mkuu wa mawasiliono, katika wakufu wa benki hiyo Karanja Nzisa, ambaye amesema benki hiyo imewekeza zaidi katika utunzi wa mazingira, kupitia upanzi wa miti na kujenga uwezo makundi yanayo endeleza shughuli hizo.
Akizungumza na wanahabari katika hafla ya upanzi wa mikoko elfu tano kule eneo la Sabaki hapa kaunti ya Kilifi, katika maadhimisho ya siku ya maji, Nzisa amesema kuwa wanashirikiana na serikali ya kitaifa, pamoja na zile za kaunti nchini, katika kufanikisha zoezi la utunzi wa mazingira na kufikia sasa, wamefanikiwa kupanda miti zaidi ya Laki nne elfu thelathini kote nchini.
Kwa upande wake mwanaharakati wa kimazingira kaunti ya Kilifi, Elphic Tosi amesema ili kuhakikisha kuwa miti hiyo inatunzwa na wanajamii, benki hiyo imeahidi kurejea eneo hilo, baada ya miezi mitatu ili kuwatuza wanajamii wakao kuwa wamelinda miti hiyo na kuhakikisha kuwa imestawi.
Aidha, mzee wa kaya katika jamii ya Mijikenda eneo hilo Edward Karisa, almaarufu Hawe Risa, amesisitiza jamii kutunza miti inayopadwa kwani itasaidia katika kuongeza idadi ya misitu, ambayo hutumika kama hifadhi ya wanyapori, ambao huvutia watalii na kuboresha uchumi wa sekta hiyo kwa jamii.

