GAVANA WA MOMBASA ATEUA BARAZA LAKE LA MAWAZIRI

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir ameteua baraza lake la mawaziri.

Katika barua rasmi iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kuwasilishwa kwenye bunge la kaunti ya Mombasa, Gavana Nassir ameteua baraza lake la mawaziri 10 huku akimteua naibu wake Francis Thoya kama waziri wa mazingira.

Daktari Mbwarali Kame Mborali ameteuliwa kuwa waziri wa elimu na masuala ya kidigitali, Evans Oanda kama waziri wa fedha na masuala ya kiuchumi, Daktari Swabah Ahmed Omar waziri wa afya na Daniel Otieno akiteuliwa kuwa waziri wa uchukuzi na miundo msingi.

Wengine ni Mahmoud Noor ambaye ameteuliwa kuwa mshauri mkuu wa gavana Nassir na pia mshauri wa masuala ya teknolojia na uvumbuzi, Kibibi Abdalla Khamis akiteuliwa kama waziri wa kilimo, mifugo na masuala ya uchumi wa raslimali za baharini na Mohamed Osman waziri wa utalii, biashara na utamaduni.