Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa bajeti Magaret Nyakang’o, imekosolewa vikali kufuatia hatua yake ya kutaka kufanya ukaguzi upya, wa matumizi ya fedha katika kaunti sita humu nchini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, ambaye pia ni Gavana wa Kaunti ya Wajir, Ahmed Abdullahi, ofisi hiyo imekuwa ikifanya ukaguzi katika kaunti zote na hivyo hatua ya kutaka kukagua upya kaunti sita, hususan kuhusu matumizi ya fedha za basari na elimu ya chekechea, bila kutoa sababu za msingi, ni kinyume cha sheria.
Abdullahi amedai kuwa suala la utoaji wa basari, limekuwa likikumbwa na ushawishi wa kisiasa na kusisitiza kuwa serikali za kaunti, zinatekeleza suala hilo kwa mujibu wa sheria na kuongeza kuwa hazina hiyo, imekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi kutoka familia zisizojiweza, na hivyo linapaswa kulindwa dhidi ya siasa na ukaguzi usio na msingi.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, ambaye pia ni Gavana wa Kaunti ya Nyeri, Mutahi Kahiga, ameongeza kuwa serikali za kaunti, zimeonyesha mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya na Kilimo sawa na elimu.

