BAADHI YA VIONGOZI KAUNTI YA KILIFI WATOA WITO KWA WAZAZI KUWA KARIBU NA WATOTO WAO WA KIKE

Viongozi wa kisiasa kaunti ya Kilifi wametoa wito kwa wazazi kaunti ya Kilifi kuchukua jukumu la kuzungumza na watoto wao wa kike kuhusiana na athari za kushiriki ngono wakiwa na umri.
Wakiongozwa na Naibu gavana wa kaunti ya Kilifi Magret Chibule, pamoja na Mwakilishi wa kike kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu, ambao walikuwa wakizungumza katika sherere za kuadhimisha siku ya vazi la jamii ya kimijikenda la kishutu katika eneo la Watamu, wamesema wazazi wanapaswa kujukumika vilivyo katika suala la malezi ya watoto wao ili kuwakinga dhidi ya kupachikwa ujauzito hali ambayo imekuwa ikichangia kushuhudiwa kwa visa vya mimba za utotoni.
Kauli hizo zimeungwa mkono na waziri wa Jinsia, Tamaduni na Michezo kaunti ya Kilifi Dama Masha, pamoja na mwenyekiti wa shirika la kutetea wanawake na watoto la Kilifi Mums Kibibi Ali, ambao wamesisitiza haja ya akina mama kuchunguza mitandao ya kijamii inayotumiwa na watoto wao na hata kutoa hamasa kwa watoto wao wa kike ili kuwalinda dhidi ya kupachikwa mimba hasa msimu wa likizo ya mwezi wa Disemba.
Kwa upande wao vijana wa shirika la KILIFI YOUTH ON THE MOVE wakiongozwa na Emily Kadzo na Jackson Wanje, wametaja hatua ya wazazi kutelekeza jukumu lao la ulezi kama mojawapo ya sababu kuu, ambazo zimechagia kwa ongezeko la mimba za utotoni kaunti ya Kilifi.