ALIYEKUWA GAVANA WA KAUNTI YA MERU KAWIRA MWANGAZA AONA GIZA HUKU NAIBU WAKE ISAAC MUTUMA AKICHUKUA NAFASI YAKE RASMI.

Siku chache baada ya mahakama kutangaza kuwa bunge la seneti lilifuata utaratibu hitajika, katika mchakato wa kumbandua aliyekuwa gavana wa Meru, Kawira Mwangaza aliyekuwa naibu wake Isaac Mutuma sasa ameapishwa rasmi.

Akizungumza mda mfupi baada ya kuapishwa, gavana Mutuma ameahidi kushirikiana na viongozi pamoja na wananchi wa matabaka mbali mbali katika kufanikisha shughuli za maendeleo kaunti hiyo, kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Aidha, amewaonya viongozi wa kaunti ya Meru dhidi ya kuendeleza tofauti zao za kisiasa na badala yake kuhakikisha kuwa wanadumisha umoja kati yao.

Ni hafla ambayo imeeandaliwa katika uwanja wa Mwendantu mjini Meru kaunti hiyo ya Meru.

Aidha, aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Kwira Mwangaza, alikuwa ameponea majaribio mawili ya kumbandua mamlakani, moja likiwa la Disemba mwaka 2022 ambapo kamati ya bunge la Seneti ilitupilia mbali madai dhidi yake.

Jaribio la pili lilijiri Novemba 2023, ambapo suala hilo lilijadiliwa na bunge zima la Seneti na akaponea baada ya kuomba msamaha.

Mara ya tatu na ya mwisho, bunge la Seneti lilikubaliana na bunge la kaunti ya Meru mwezi Agosti mwaka 2024 na kumwondoa afisini kwa makosa mbalimbali.