ABDULSWAMAD AWATAKA WABUNGE NA MASENETA KUSHUGHULIKIA MRADI WA GALANA KULALU

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amewataka wabunge na maseneta kuhakisha wanashugulikia suala la ardhi ya Galana Kulalu ili irejee kwa serikali ya kaunti kwa minajili ya kuwafaidi wananchi katika uzalishaji wa chakula, hatua ambayo itasaidia kudhibiti baa la njaa ambalo limekuwa likishuhudiwa kanda ya pwani na nchini Kote.
Akizungumza katika eneo la Ganze kaunti ya Kilifi Nassir amesema iwapo watatekeleza hilo itakuwa afueni kwa wenyeji wa pwani na nchini kote kwani hawatakabiliwa na baa la njaa tena siku za usoni.
Aidha, amewataka magavana wote wa Pwani kushirikiana na masharika mengine ili kuweka miradi ya unyunyuzaji maji eneo la Galana Kulalu kwa manufaa ya wakaazi wa kaunti ya Kilifi ambayo wenyeji wengi wamekumbwa na baa la njaa.
Kwa upande wake Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedeon Mung’aro amesema wanashirikiana na serikali kuu kuhakikisha chakula Cha msaada kinasambazwa katika maeneo yaliyoathirika na baa la njaa Kaunti ya Kilifi na pia wanapania kuandaa kongamano la viongozi wa Jumuiya ya kaunti za pwani ili kuweka mikakati ambayo itasaidia kudhibiti changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili mara kwa mara wenyeji wa pwani.
Naye mbunge wa Kaloleni kaunti ya Kilifi Paul Katana ameitaka serikali kufanya uchunguzi na kuwakabili waliohusika katika kulemaza mradi wa Galana Kulalu kwa kufuja fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuufanikisha.