BUNGE LA KAUNTI YA TAITA TAVETA LAADHIBU WAWAKILISHI WADI WAWILI KWA KUWAONDOA MAMLAKANI.

Kaimu Spika wa bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime ametangaza viti vya wawakilishi wadi ya Mboghoni mjini Taveta na Wadi ya Rong’e mjini Mwatate kuwa wazi.

Kulingana na Mwadime, wawakilishi wadi hao ambao ni Dorcus Mlughu na Khalifa Taraya, wamekosa kuhudhuria vikao vinane vya bunge, hivyo hawapaswi kuendelea kuwa wanachama wa bunge hilo kisheria.

Mwakilishi wadi ya Mboghoni mjini Taveta, Khalifa Taraya, ameitaja hatua hiyo kuwa kinyume Cha Sheria, akidokeza kusaka usaidizi wa kisheria, kuhusiana na mamuuzi hayo, kwani hakuna kosa lolote walilofanya, linalo stahili adhabu hiyo.

Ikumbukwe kwamba kaimu spika Anselim Mwadime, aliapa kuwaadhibu vikali wajumbe hao, Kwa madai ya kukiuka Sheria za bunge, baada ya kueleza kutoridhishwa kwao na jinsi bunge hilo, linavyoendesha shughuli zake.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Mwakilishi wadi ya Kaloleni mjini Voi Ahzar Din, kuomba msamaha bungeni, jambo lililoyumbisha msimamo wa awali wa  wawakilishi hao.