RAIS WILLIAM RUTO APONGEZA USHAURI WA RAILA ODINGA KWA VIONGOZI WA SERIKALI KUU.

Rais William Ruto amesema serikali inajivunia mawazo yenye hekima, maono na maoni, yaliyotolewa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, wakati wa hotuba yake kwenye mkutano wa tatu wa kitaifa, wa Baraza la Mawaziri ulioandaliwa Karen, jijini Nairobi.

Kupitia ukurasa wake wa X leo Ijumaa, Rais Ruto amesema, wito wa Raila kwa viongozi waangazie yaliyo mema, baadala ya kutaka umaarufu, unaambatana na malengo ya serikali yake.

Amesema serikali imepata mafunzo mengi kutoka kwa Raila, kuhusu utekelezaji wa miundombinu ya kitaifa, ikiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, ujenzi wa masoko ya mazao ya kilimo na upanuzi wa viwanja  vya ndege, miongoni mwa miradi mingine.

Kwa upande wake aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, ametoa wito kwa Wakenya, kuweka mbele udhabiti wa taifa, huku akiwataka viongozi wa serikali, kuhakikisha sera za serikali, mipango na maamuzi zingatia maslahi ya wakenya wote.

Akizungumzia mkataba kati ya chama cha  ODM na UDA, Raila amesema mkataba huo, ambao ulisababisha kubuniwa kwa serikali jumuishi, chini ya uongozi wa Rais William Ruto mwaka jana, ulilenga kuimarisha udhabiti wa taifa hili.

Akipigia debe umoja wa kitaifa, kiongozi huyo wa chama cha ODM, amedokeza kuwa taifa ambalo limegawanyika, haliwezi timiza mageuzi yoyote.

Aidha, ametoa changamoto kwa viongozi wa serikali, kuhakikisha umma haunufaiki tu na mipango ya serikali, lakini pia unajumuishwa katika kubuni sera na utekelezwaji wake.