WALIMU 482 KAUNTI YA GARISSA WAKOSA KUPANDISHWA CHEO NA TUME YA KUAJIRI WALIMU NCHINI TSC.

Muungano wa walimu KNUT kaunti ya Garissa umekashifu vikali hatua ya tume ya kuajiri walimu nchini TSC, kubatilisha hatua ya kupandisha vyeo walimu 482.

Katibu wa muungano huo kaunti hiyo Abdilrazak Hussein, amesema hatua hiyo imevunja moyo walimu katika kuendeleza kazi zao kaunti hiyo, ikizingatiwa kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama.

Hussein amesema kuwa idadi kubwa ya walimu kaunti hiyo, wamekuwa wakifanya kazi katika ngazi moja pasi na kupandishwa cheo, jambo ambalo anataja kudhihirisha kuwa, wametengwa na serikali ya kitaifa.

Akielezea gadhabu ya walimu hao, katibu huyo amesema kuwa kupandisha walimu vyeo katika eneo hilo, ni njia mojawapo ya kuwapatia motisha kufanikisha majukumu yao kwa wanafunzi wa jamii zilizoko kaunti hiyo.