RAIS WILLIAM RUTO AFANYA KIKAO NA VIONGOZI WA PWANI KATIKA IKULU YA NAIROBI.

Kuna haja ya serikali ya kitaifa kuweka mikakati ya kuboresha mapato na utendakazi wa bandari ya Mombasa.

Haya ni kwa mujibu wa rais William Ruto ambaye amesema kuwa bandari ya Mombasa, inauwezo mkubwa wa kupatia taifa hili mapato mengi zaidi na hata kusaidia wananchi wengi kupata nafasi za ajira.

Akizungumza katika kikao na viongozi waliochanguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye bunge la kitaifa na lile la seneti pamoja na mawaziri, rais Ruto ametoa wito wa viongozi hao kuunga mkono ajenda ya serikali yake katika kuboresha miundo msingi ya uchumi na maendeleo eneo la Pwani.

Mawaziri waliohudhuria kikao hicho wakiongozwa na waziri wa uchumi wa bahari na maziwa nchini Ali Hassan Joho pamoja na waziri wa michezo na vijana Salim Mvurya wamemuhakikishia rais kuwa watatekeleza majikumu aliyowapatia ili kuboresha uongozi wake.

Kwa upande wake seneta wa kaunti ya Kilifi, Steward Madzayo amesema kuwa ni wakati wa wakaazi wa Pwani kufaidi matunda ya kuunga mkono serikali kuu huku mbunge wa Likoni, kaunti ya Mombasa Mishi Mboko akimtaka rais kupuuza viongozi wanaompinga.