RAIS WILLIAM RUTO AZURU ENEO LA MLIMA KENYA.

Rais William Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya siku nne eneo la mlima Kenya kuanzia siku ya Jumanne hadi Ijumaa, ambapo atakagua miradi kadhaa ya maendeleo.

Ziara hiyo, itakuwa ya kwanza kwa Rais katika eneo hilo, miezi sita tangu amtimue aliyekuwa Naibu Rais wake Rigathi Gachagua, anayetoka eneo hilo.

Aidha, Rais atatumia ziara hiyo kujipigia debe na kutafuta uungwaji mkono kutoka eneo hilo, katika azma ya kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Rais atazindua miradi kadhaa ya maendeleo eneo hilo na kukagua miradi mingine iliyoanzishwa chini ya mfumo wake wa uchumi wa Bottom Up.

Miongoni mwa miradi atakayozindua Rais, ni pamoja na ile ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu, uunganishaji umeme, usambazaji maji na unyunyiziaji mashamba maji, miongoni mwa miradi mingine.

Kiongozi wa nchi ameratibiwa kuzuru kaunti tisa za mlima Kenya, ikiwa ni pamoja na Laikipia, Nyeri, Meru, Kirinyaga, Nyandarua, Murang’a, Embu, Tharaka-Nithi na Kiambu.