WAKENYA WATAKIWA KUDUMISHA AMANI NA UMOJA.

Rais William Ruto amesisitiza haja ya viongozi wa kisiasa katika taifa hili kushirikiana kwenye ujenzi wa taifa.

Kiongozi huyo wa taifa amesema kuwa licha ya viongozi hao kuwa na msimamo tofauti ya kisiasa, kuna haja yao kuhakikisha kuwa wanahubiri amani katika maeneo yote ya taifa hili.

Akizungumza hapo jana, baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa la AIC Jericho kule kaunti ya Nairobi, amewataka wakenya kwa jumla kujitenga na masuala ya ukabila na kudumisha umoja.

Vile vile rais Ruto, amewahakikishia wakenya kuwa serikali yake itashirikiana na viongozi wa kisiasa, pamoja na wale wa kidini katika kufanikisha ajenda ya serikali yake.