IDARA YA USALAMA YATANGAZA KAFYU KAUNTI YA LAMU.

Idara ya usalama kaunti ya Lamu imetangaza marufuku ya wananchi kukusanyika kwenye mikutano na shughuli zozote, kuanzia saa mbili usiku, kwa takriban mwezi mmoja kuanzia leo.

Akitoa marufuku hiyo, kamishna wa kaunti hiyo Wesley Koech, amesema kuwa hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa mashambulizi ya siku ya jumamosi iliyopita, mwendo wa saa kumi na mbili jioni katika kijiji cha Mangai kaunti hiyo.

Kamishna Koech amesema kuwa miongoni wa mikutano iliyopigwa marufuku, ni ile ya ibada za usiku kwenye makanisa na misikiti, pamoja na sehemu za burudani kaunti hiyo.

Koech amesema kuwa idara ya usalama, imechukua muelekeo huo baada ya kubaini kuwa idadi kubwa ya visa hivyo, hufanyika msimu huu wa mwezi wa ramadhani.