WANAHABARI KAUNTI YA TAITA TAVETA WAANDAMANA DHIDI YA WAZIRI WA AFYA KAUNTI HIYO.

Wanahabari kaunti ya Taita Taveta wamefanya maandamano ya amani kupinga matamshi ya waziri wa afya wa kaunti hiyo Gifton Mkaya, wakiyataja kuwa ya vitisho, uongo na yenye njama ya kuharibu sifa ya vyombo vya habari.

Wanamshutumu waziri Mkaya, kwa kudai kuwa waandishi wa habari wamekuwa wakidai pesa, ili kuangazia sekta hiyo ya afya, ambayo imezidi kudorora tangu achukue hatamu ya uongozi kwenye wizara hiyo.

Wakiongozwa na kaimu mwenyekiti wa muungano wa waandishi wa habari kaunti hiyo Sylvester Kituku, wamesema kuwa hasira za waziri huyo wa serikali ya kaunti ya Taita Taveta, zinatokana na wanahabari kufichua uozo uliopo kwenye sekta ya afya kaunti ya Taita Taveta.

Ni Kauli ambayo imeungwa mkono na mmoja wanahabari hao Hezron Kimari, ambaye amesema kuwa juhudi zao za kutaka kufanya mazungumzo na serikali ya kaunti hiyo, zimekuwa zikiambulia patupu huku baadhi ya viongozi kwenye serikali ya kaunti ya Taita Taveta, wakipuuza wito wa waandishi hao.