Baraza la maimamu na wahubiri wa kiislamu nchini CIPK sasa linaitaka serikali kuondoa ushuru wa tende, wakati wa mwezi wa ramadhan, unaotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
Kulingana na mwenyekiti wa baraza hilo kitaifa Sheikh Ibrahim Abdallah Ateka, lengo kuu la mataifa ya kiarabu kutuma tende, ni kutoa msaada kwa waumini wa dini hiyo, wasiokuwa na uwezo wa kumudu bei yake na wala sio kufanikisha shughuli za kibiashara.
Akizungumza na wanahabari kaunti ya Mombasa, Sheikh Ibrahim amesema kuwa kuondolewa kwa ushuru wa bidhaa hiyo, kutaleta afueni kwa jamii za waumini wa dini hiyo, ambao watakuwa wakishiriki mfungo wa ramadhani.
Kauli yake imeungwa mkono na katibu mkuu wa baraza hilo Sheikh Muhammad Khalifa, ambaye amemtaka rais William Ruto, kuzingatia ombi lao kwa kipindi cha msimu wa ramadhani pekee.

