EUGENE WAMALWA ASEMA HUENDA CHAMA CHA ODM KIKASAMBARATIKA.

Kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa, amesema kuwa chama chake kitaendelea kusalia upande wa upinzani, ili kuwajibisha utendakazi wa serikali ya Rais William Ruto.

Wamalwa amewasuta viongozi wa chama cha ODM, kutokana na mgawanyiko ambao umeendelea kushuhudiwa ndani ya chama hicho, baada ya baadhi ya viongozi kuteuliwa kuhudumu kwenye baraza la mawaziri ndani ya serikali kuu.

Akizungumza katika kaunti ya Busia, Wamalwa amesema anakisia kuvunjika kwa chama cha ODM, iwapo viongozi hao wataendelea kuunga mkono serikali ya Kenya kwanza.

Wakati uo huo, Wamalwa amemshutumu rais William Ruto, kwa kujaribu kumaliza shughuli za upinzani haswa eneo la Magharibi mwa Kenya, kwa kuunganisha vyama vya kisiasa na kushawishi vinara wa vyama hivyo kujiunga na chama chake cha UDA.