Waziri wa utumishi wa umma Justine Bedan Njoka Muturi, ameendeleza shutuma zake dhidi ya serikali anayotumikia, kwa madai ya kutozungumzia masuala ya utekaji nyara wa vijana katika taifa hili.
Kulingana waziri Muturi, serikali ya Kenya Kwanza iliahidi wakenya kusitisha visa vya mauaji ya kiholela na utekaji nyara, wakati wa kampeni za kuwania uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na sharti itemize ahadi hiyo.
Katika kikao na waandhishi wa habari, Muturi amelaani vikali mauaji ya vijana, waliotekwa nyara na mwaka jana katika eneo la Mlolongo na kisha kupatika wakiwa wameaga, na kusema kuwa sio jambo la kufurahisha kuona familia zao, zikiomboleza kwa zaidi ya mwezi mmoja pasi na ufahamu wa waliko wapendwa wao.
Muturi aidha amepinga madai ya maafisa wa polisi nchini Kenya, kutokuwa na ufahamu kuhusiana na visa hivyo huku akimtaka rais William Ruto, kutoa amri ya kusitishwa kwa visa vya mauaji na utekaji nyara wa wakenya, kama alivyoahidi wakati wa kampeni za kuwania urais mwaka 2022.

