SERIKALI YA KAUNTI YA NAIROBI YAAHIDI KUJENGA SOKO ENEO LA SOUTH B.

Serikali ya kaunti ya Nairobi itajenga soko jipya eneo la South B kaunti ya Nairobi, ili kuwaondoa wachuuzi ambao wamekuwa wakifanyia biashara zao kando kando mwa barabara.
Ujenzi huo wa soko unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 350.

Akihutubia wafanyabiashara katika eneo hilo, mwakilishi wadi hiyo ya South B, Waithera Chege amesema kuwa hatua hiyo inalenga kukabiliana na changamoto za ajali, zinazo husisha wachuuzi ambao wamekuwa wakiendeleza bishara zao kando ya barabara za wadi hiyo.

Chege vile vile ameongeza kuwa sharti wafanyabiashara hao, wapate mazingira bora ya kuendeleza shughuli zao katika wadi hiyo, ili kuboresha maisha yao kiuchumi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa idara ya masoko kaunti ya Nairobi, David Githaiga amesema kuwa tayari serikali ya kaunti hiyo, imetoa notisi ya ujenzi wa soko hilo kwa wafanyabiashara hao huku mwenyekiti wa wafanyabiashara hao James Maina, akipongeza hatua hiyo kwa kile anachosema idadi kubwa ya wachuuzi eneo hilo, wamepoteza maisha baada ya kugongwa na magari na pikipiki, wanapokuwa wakifanya biashara zao.