Wakenya wameendelea kusisitizwa kujisaji kwenye bima mpya ya SHA, ili kusaidia serikali kuendeleza mipango ya kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa mujibu wa rais William Ruto, serikali ya kitaifa inategemea pakubwa deta za wizara ya afya, hasa kuhusiana na idadi ya wakenya katika maeneo mbali mbali ya taifa, ili kuboresha miundo msingi ya afya.
Akizungumza katika kaunti ya Kakamega, Ruto amewaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kuwahadaa wananchi, kuhusiana na mpango huo, kwa kile alichosema lengo kuu la serikali kuanzisha bima hiyo mpya ya SHA, ni kusaidia wananchi kupata huduma bora za afya kwa gharama ya chini zaidi.
Aidha, Ruto amesisitiza kuwa ujio wa mbima mpya humu nchini ni njia mojawapo ya kuleta usawa kati ya wakenya wa matabaka mbali mbali katika suala la utoaji wa huduma za afya.
Ni kauli ambayo imeungwa mkono na spika wa bunge la kitaifa Moses Masika Wetangula, ambaye amesisitiza wananchi kusajiliwa kwenye bima hiyo.
Semi hizo zimejiri baada ya mbunge wa Mumias Mashariki kaunti ya Kakamega, Peter Salasya kudai kuwa mfumo wa SHA umekuwa ukitesa wakenya kwenye taasisi za afya nchini.

