Mahakama ya Malindi kaunti ya Kilifi imemuachilia huru mhubiri tata Paul Mackenzie na washtakiwa wengine 8 waliokuwa wameshitakiwa pamoja naye.
Jaji wa mahakama hiyo Ivy Wasike, ambaye pia ni naibu msajili wa mahakama hii ya Malindi, amesema kuwa mahakama haina uwezo wa kuwapa dhamana washukiwa hao na kisha kufunga mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao.
Hii ni baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo kuyaondoa mashtaka yanaowakabili washukiwa hao na kutaka wafunguliwe mashtaka mengine mapya ya ugaidi katika mahakama ya Shanzu ambayo inahusika na kesi dhidi ya ugadi.
Kwa upande wake wakili wa Mackenzie, Elisha komora, amesema kuwa mahakama ya Malindi haiwezi kumzuilia tena Mackenzie pamoja na washukiwa wengine, baada ya muda wa kuzuiliwa kwao kukamilika.
Aidha Mackenzie amekamatwa tena muda mfipi baada ya kuachiliwa huru na mahakama hiyo na kuchukuliwa na maafisa wa polisi huku akitarajiwa kufunguliwa mashtaka ya ugaidi katika mahakama ya Shanzu.

